Kuanzishwa kwa TANU katika Majimbo:

.....Wasomi wa Makerere, ambao Mwangosi aliwaamini sana katika kuunda TANU,  walipopata habari kuhusu mkasa wa Taratibu na DC, Bwana Smith, waliogopa.  Waliamua kujiweka mbali kabisa na mambo ya siasa na kuendelea na kazi yao ya  kufundisha. Haruna Taratibu na Omari Suleiman sasa waliamua kugeuza mbinu,  waliitisha mkutano wa siri usiku nyumbani kwa Swedi bin Athumani.   Mkutano huu uliamua kuwa Taratibu lazima aende makao makuu ya TANU Dar es  Salaam akazungumze na Nyerere ana kwa ana kuhusu matatizo yaliyokuwa  yakiikabili TANU Dodoma. Mahdi Mwinchumu aliyekuwa mwanachama wa TANU Dar es  Salaam alijitolea kufuatana na Taratibu hadi makao makuu ya chama Dar es  Salaam kwa kuwa alikuwa akijuana na viongozi wa TANU. Said Mussa mjumbe  mwingine wa ile kamati ya siri alijitolea vilevile kufuatana na Taratibu na  Mwinchumu hadi Dar es Salaam.   

Siku ya kuondoka Job Lusinde alikwenda stesheni ya gari moshi kuagana na ule  ujumbe uliokuwa ukielekea Dar es Salaam, makao makuu ya TANU. Lusinde  aliuambia ule ujumbe kuwa jamaa wa Makerere wanaunga mkono maamuzi yote  yatakayoamuliwa na ile kamati ya siri.   Kwa bahati nzuri katika gari moshi lile lile ambamo Taratibu na wenzake  walikuwa wakisafiri kulikuwa na wajumbe wa TANU kutoka Kigoma, Bukoba na  Mwanza wakisafiri kwenda Dar es Salaam kuhudhuria mkutano mkuu wa kwanza wa  mwaka wa TANU.   Wahudumu ndani ya gari moshi walipofahamu kuwa walikuwa na wajumbe wa TANU  kwenye gari moshi lile, waliwafanyia heshima kubwa. Mmoja wa wahudumu wale  alijitolea kumpa malazi Salum Mussa nyumbani kwake Dar es Salaam. Mahdi  Mwinchumu aliwapeleka Haruna Taratibu na Said Mussa makao makuu ya TANU New  Street ambako walifanya mazungumzo na Nyerere pamoja na Rupia. Uongozi wa  makao makuu ulielezwa kwa ufupi matatizo yaliyokuwa yakikabili Dodoma katika  kufungua tawi la TANU. Papo hapo Nyerere alimwalika Taratibu kuhudhuria  mkutano mkuu Hindu Mandal Hall kama mjumbe wa Jimbo la Kati. Mkutano ule  ulimchagua Taratibu kuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya Taifa ya TANU. Taratibu na  ujumbe wake walirudi Dodoma washindi, walikwenda Dar es Salaam watu  wasiojulikana na walirudi nyumbani wakifuatana na mjumbe wa Kamati Kuu ya  Taifa wa TANU, chombo cha juu kabisa katika chama. Nyerere alimpa Taratibu  dafari ya tasjili ya wanachama, kadi mia moja hamsini za uanachama wa TANU  na nakala hamsini za *Bill of Rights.*   

Kazi ya kuwahamasisha na kuwaingiza watu TANU alipewa Omari Suleiman, na  fundi cherahani mwingine aliyejulikana kwa jina la Abdu Mohamed Mkamba. Mara  tu baba mwenye nyumba wake alipopata habari za kuwa mpangaji wake, Haruna  Taratibu alikuwa mwanachama wa TANU, alimfukuza kutoka kwenye nyumba yake.   Baada ya kupata kikundi kidogo cha wanachama, Taratibu alipiga simu makao  makuu ya TANU na kuzungumza na kaimu katibu, Elias Kissenge akaomba ruhusa  ya kufanya uchaguzi. Kissenge hakuweza kutoa uamuzi wowote wa maana kuhusu  tatizo la uongozi wa TANU Dodoma.   Taratibu alifanikiwa kumpata Kambona ambae aliidhinisha uchaguzi ufanyike  kwa shuruti moja la kuwa Hassan Suleiman na Ali Ponda waruhusiwe kushiriki  na kugombea uongozi wa chama. Kusisitiza kwa Kambona juu ya uongozi wa  zamani wa TAA kuongoza chama kipya huenda kulishawishiwa na mafanikio ya  zamani ya uongozi wa Hassan Suleiman mbae alimfahamu huko Dodoma wakati  Kambona alipokuwa mwalimu akifundisha Kikuyu Secondary School.   Kwa bahati mbaya, wanachama wa TANU waliokuwa wanainukia na chama pale mjini  Dodoma waliwaona Hassan Suleiman na Ali Ponda kama wasaliti kutokana na  kutokushirikiana na wenzao katika kuanzisha TANU.   Wakati ametatizwa na tatizo la uchaguzi wa TANU, Taratibu alijulishwa na  makao makuu kuwa makamo wa rais, John Rupia, atapita Dodoma kwa gari moshi  akiwa njiani kwenda Tabora kushughulikia mambo ya chama. Gari moshi  liliposimama Dodoma Rupia alishangazwa kuona kundi la wananchama wa TANU  wakimsubiri katika kituo cha gari moshi wakimtaka avunje safari waende mjini  kujadili na kutatua tatizo la uchaguzi. Rupia aliwaeleza wanachama wa TANU  wa Dodoma kuwa yeye hakuwa na idhini kutoka makao makuu kufanya shughuli  yoyote ya chama mjini Dodoma. Wanachama wa TANU hawakutaka kusikia lolote na  walimwambia Rupia kuwa wamechoshwa na makao makuu kwa kushindwa kwake kutoa  uamuzi wa tatizo la uchaguzi. Mizigo ya Rupia ilishushwa chini kutoka kwenye  gari moshi na Rupia akawa hana khiyari isipokuwa kuwafuata wale wanachama wa  TANU hadi mjini.   Ghafla mji mzima ukavuma tetesi kuwa makamu wa rais wa TANU, John Rupia,  yupo mjini kufungua tawi la TANU.

Rupia alimwita Hassan Suleimna na akamtaka  alete hati ya tasjili ya TANU Hindu Mandal siku inayofuata, mahali ambako  mkutano utafanyika. Hassan Suleiman hakutokea mkutanoni lakini alimtuma mtu  apeleke ile hati. Ali Ponda alihudhuria mkutano ule. Rupia alikuwa  mwenyekiti wa mkutano na TANU ikafanya uchaguzi wake wa kwanza. Alexander  Kanyamara alichaguliwa Rais; Haruna Taratibu Makamu wa Rais, Abdu Mohamed  Mwamba, Katibu na Omari Suleiman Mweka Hazina.   Miongoni mwa wanachama waasisi alikuwa mwanamke mmoja wa Kimanyema, Binti  Maftah Karenga; wengine walikuwa Bakari Yenga, Maalim Khalfan, mwanachuoni  wa Kiislamu aliyekuwa akiheshimawa sana, Idd Waziri na Said Suleiman. Wale  wasomi wa Makerere hata mmoja hakujitokeza kwenye mkutano huu wa kuasisi  TANU. Ali Ponda, mwanasiasa mkongwe alipuuzwa na hakuchaguliwa kushika  wadhifa wowote. Walipoona hawakupewa wadhifa wowote katika TANU, Ali Ponda  na Hassan Suleiman walijiunga na UTP kuipinga TANU.   Baada ya uchaguzi huo, wale mafundi cherahani wawili, Abdu Mohamed Mkamba na  Omari Suleiman, walianza kuhamasisha wananchi wazi wazi kujiunga na TANU ili  wapiganie uhuru wa Tanganyika.   Tawi la TANU la Dodoma baada ya kujizatiti pale mjini, lilituma wanaharakati  kuwahamasisha watu wa Kondoa ili wafungue tawi la TANU katika wilaya hiyo.  Abdallah Jumbe alizipenyeza kadi za TANU na kuzipeleka kwenye wilaya hiyo  kwa siri akaanza kuandikisha watu.   D.C. wa Singida alikuwa jeuri sana kiasi kwamba ni baada ya Mkutano Mkuu wa  Tabora wa mwaka 1958 ndipo Abdallah Jumbe aliweza kufanikiwa kufungua tawi  mjini Singida. Wakati huo TANU ilikuwa na nguvu sana ikiwa na wajumbe wake  katka Baraza la Kutunga Sheria. Kwa ajili hii hakuna Mzungu aliyethubutu  kuwa fedhuli kwa TANU na kuwabughudhi wanachama wake.   *Jimbo la Kusini, 1955*   TAA mjini Lindi ilikuwa chini ya uongozi wa Suleiman Masudi Mnonji aliyekuwa  Rais na Katibu wake alikuwa Mohamed Waziri. Mnonji alikuwa fundi cherahani  na Waziri alikuwa mchoraji wa ramani za nyumba. TAA ilichelewa kuanza mjini  Lindi. TAA ilianzishwa Lindi mwaka 1953 wakati uongozi wa TAA mjini Dar es  Salaam si tu ulikuwa unaigeuza TAA kuwa chama cha siasa bali ulikuwa  ukifanya mipango kumpeleka mjumbe wake Umoja wa Mataifa kudai uhuru. Masudi  Mnonji alikuwa na uzoefu wa kutosha katika siasa.   Baada ya Vita Kuu ya Pili alikuwa amejaribu kuanzisha vyama vya wafanyakazi  katika mashamba mbalimbali ya mkonge kusini mwa Tanganyika. Vilevile  aliwakusanya wapishi na madobi mjini Lindi waanzishe umoja wao. Ilikuwa  kupitia juhudi zake binafsi TAA ijapokuwa ilichelewa, ilikuja kuanzishwa  mjini Lindi na Mnonji alijitolea nyumba yake katika mtaa wa Makonde kama  ofisi ya chama. Mnonji kwa kutambua umuhimu wa kuwa na uongozi ulioelimika  vizuri, alimleta Nangwanda Sijaona kutoka Nachingwea aje aishauri TAA jinsi  ya kufanya mambo kwa utaalamu.   Wakati huo mjini Lindi kulikuwa na chama cha wafanyakazi bandarini  Dockworkers' Union chini ya uongozi wa Mussa Athumani Lukundu, chama ambacho  kwa kiasi chake kilianzisha vuguvugu la siasa za vyama vya wafanyakazi.   Ingawa vyama hivi viwili, yaani TAA na Dockworkers' Union vilikuwepo katika  mji mmoja, siasa za hiki chama cha pili cha wafanyakazi bandarini  hazikupitia TAA kama ilivyokuwa mjini Dar es Salaam. Hii kidogo ilidhoofisha  mwamamko wa siasa kwa wananchi. Jimbo la Kusini lilikuwa katika usingizi  mzito wakati sehemu nyingine Tanganyika zilikuwa zikipiga hatua kwenda mbele  zikiandaa vita dhidi ya utawala wa kikoloni. Chanzo cha usingizi huu mzito  huko kusini ulikuwa na asili yake katika historia ya Tanganyika.   Vita vya Maji Maji vilipoanza kusini ya Tanganyika mwaka 1905 kwa nia ya  kuwafukuza Wajerumani kutoka Tanganyika, zile sehemu zenye Wakristo wengi  zilikataa kujiunga na vita na badala yake wakajiunga na majeshi ya  Wajerumani na kupigana bega kwa bega na dhidi ya wazalendo. Hii ilitokana na  sababu ya kuwa uasi dhidi ya dhulma wa Wajerumani ulianza katika maeneo  yenye Waislamu wengi na vita vikachukua sura ya vita vya Kiislamu dhidi ya  Wazungu ambao dini yao ni Ukristo. Kwa kuwa wamishonari walikuwa washirika  wa wakoloni, walichukuliwa kama maadui na hivyo ikawa vituo vyao  vinashambuliwa na wapiganaji wa Maji Maji. Kutokana mashambulizi haya,  Wakristo walivichukua Vita Vya Maji Maji kama vita dhidi ya Ukristo.   

Harakati za Maji Maji zilishindwa na Wajerumani walifanya fisadi kubwa dhidi  ya wananchi na viongozi wao. Jambo hili liliacha kovu kubwa katika fikra za  wananchi na kwa upande wa Wakristo ambao walinusurika na ghadhabu ya  Wajerumani, wengi wao wakajiweka mbali na aina yoyote ya kupinga ukoloni.   Kufuatia historia hii Waafrika waliokuwa kusini ya Tanganyika sasa wakiwa  chini ya utawala wa Waingereza na kuwa chini ya himaya ya wamishonari  walipupazwa kiasi kiasi kwamba waliogopa siasa.   Baada ya Waafrika kushindwa vita kwa silaha kali za Wazungu sasa Kanisa  likaona ndani ya fadhaa ile fursa yao kutawala sehemu hiyo kwa kutoa  vishawishi kama vile shule na hospitali. Kwa hiyo Wamishionari na Waingereza  walionekana kama mabwana wema wenye kuwajali raia zao kinyume na serikali  katili na ya kidhalimu ya Wajerumani.   Vuguvugu la siasa kama ilivyokuwa Vita vya Maji Maji, lilianza katika maeneo  ya Waislam kufuatia mfumo ule ule kama ilivyokuwa katika upinzani wa ukoloni  wa Wajerumani. Wakristo katika Jimbo la Kusini waliiona TANU kama  walivyoviona Vita Vya Maji Maji, kama harakati nyingine za Waislam  zilizokuwa zikija tena kwa mara ya pili kuvuruga amani na utulivu. TANU  ilipoanza ikawa inavuma kuwa safari hii Waislam walikuwa wamemua kuanzisha  vita dhidi ya Waingereza kama walivyoanzisha vita na Wajerumani.   TANU ilipoanzishwa mjini Dar es Salaam na hisia za utaifa zilipokuwa  zikipanda pole pole katika fikra za wananchi katika sehemu nyingi za  Tanganyika, Jimbo la Kusini lilikuwa bado usingizini likiishi katika zama za  kale. Mnonji na Waziri, kwa sababu ya utu uzima wao, daraja yao katika jamii  na hasa kutokana na kuhusika kwao katika siasa za pale mjini, walikuwa na  nguvu kubwa katika TAA. Wakati TANU imeshachukua nafasi ya TAA, uongozi wa  TAA Lindi haukutaka kufungua tawi la TANU.   Mtu wa kwanza kuutanabaisha uongozi wa TAA mjini Lindi juu ya mageuzi  yaliyokuwa yakitokea Tanganyika na kuanzishwa kwa chama kipya cha siasa  mjini Dar es Salaam alikuwa Abdallah Juma Makopa, kijana kutoka Tanga  akifanya kazi ya ukarani Posta ya Lindi.

Makopa aliwaendea Mnonji na Waziri  na kuwajulisha kuhusu kuanzishwa kwa TANUmjini Dar es Salaam na aliwashauri  waanzishe TANU pale Lindi. Jambo hilo lilipingwa moja kwa moja na Mnonji,  Waziri, Said Nassoro, Abdallah Mhuji na wanachama wengine wa TAA.   Chama cha Waafrika ambacho kilianzishwa siku nyingi mjini Lindi na kwa  hakika ndicho kilikuwa chama cha pekee kushughulikia maslahi ya Waafrika  sehemu za kusini kilikuwa African Welfrare Association ambacho mlezi wake  alikuwa John Nevi, Mjaluo kutoka Kenya na katibu wake alikuwa Casian Njunde,  Mngoni wa Songea. Makopa aliposhindwa kukishawishi kile kikundi cha wazee wa  TAA aliwaendea Yusufu Chembera na Rashid Salum Mpunga. Chembera alikuwa na  umri wa miaka thelathini na nne na Mpunga alikuwa kijana wa miaka ishirini  na saba. Chambera alikuwa amesoma hadi shule ya msingi na Mpunga alikuwa  amemaliza madras. Chembera alikuwa akifanya kazi katika kantini ya Lindi Welfare Centre, wakati Mpunga alikuwa dereva wa lori aliyeajiriwa na mfanyabishara wa Kihindi. Makopa aliwashauri Chembera na Mpunga juu ya  uwezekano wa kuwahamasisha wananchi wawaunge mkono ili tawi la TANU  lifunguliwe pale mjini. Aliwaambia alitaka sana kufanya hivyo yeye mwenyewe  lakini asingeweza kwa sababu yeye alikuwa mtumishi wa serikali na hakuwa  akifahamika sana mjini. Uongozi kama wao ndiyo ungeweza kuaminiwa na  wananchi na usingetiliwa mashaka. Makopa, Chembera na Mpunga walikubaliana  kuwa kabla ya kuanza kufanya kampeni waziwazi kwa ajili ya TANU, lazima  wawaandikishe wanachama wachache kama waasisi wa chama. Mpunga na Chembera  walimwandikisha kijana mmoja akiitwa Abdallah Faraj na katika muda mfupi  waliweza kuwapata takriban...